Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
ameiomba Jamhuri ya Watu wa China kusaidia mipangomiji katika baadhi ya
maeneo ya kimkakati ya Tanzania na China imekubali kuleta timu ya
wataalam kufanya tathmini katika maeneo hayo yote ama baadhi ya maeneo
hayo ili kujua mahitaji kamili ya mipangomiji ya maeneo hayo.
Rais
Kikwete alitoa ombi hilo, Jumapili, Januari 12, 2014, wakati
alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nyumba, Makazi na
Maendeleo ya Mjini na Vijiji wa China, Mheshimiwa Jiang Weixin,
mazungumzo yaliyofanyika Ikulu, Zanzibar.
Rais
Kikwete alikuwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu Tanzania Visiwani
ambako alishiriki katika Sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar
wakati Mheshimiwa Weixin alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Watu wa China
Mheshimiwa Xi Jinping katika sherehe hizo.
Katika
mazungumzo hayo, Rais Kikwete alimweleza Mheshimiwa Weixin kuhusu
juhudi zinazofanywa na Serikali kuhusu umuhimu wa upangaji miji na
kuiweka miji ya Tanzania katika hali nzuri akisisitiza kuwa Serikali
inakabiliwa na changamoto za ukosefu wa uwezo wa kiufundi, ukosefu wa
vifaa na ukosefu wa uwezo wa kifedha ili kuifanya kazi hiyo kwa
ufanisi..
Rais
Kikwete amesema kuwa pamoja na kwamba changamoto za mipangomiji ziko
katika miji yote ya Tanzania, ikiwamo Dar Es Salaam, lakini Serikali kwa
sasa inapenda kuelekeza nguvu zake katika miji mitatu ambayo ina uwezo
mkubwa wa kuendelea kwa kasi kubwa zaidi katika miaka michache ijayo na
hivyo lazima iendelee ikiwa imepangwa vizuri.
Rais Kikwete ameitaja miji hiyo mitatu kuwa ni mji mpya wa Kigamboni, Dar es Salaam na miji ya Mtwara na Lindi ambayo kwa sababu ya uvumbuzi wa gesi na uchumi utakaotokana na uvumbuzi huo, inayo uwezo mkubwa wa kupanuka na kukua kwa haraka na isipopagiliwa vizuri kutokea mwanzo inaweza kuishia ikipanuka kwa ujenzi holela.
Rais Kikwete ameitaja miji hiyo mitatu kuwa ni mji mpya wa Kigamboni, Dar es Salaam na miji ya Mtwara na Lindi ambayo kwa sababu ya uvumbuzi wa gesi na uchumi utakaotokana na uvumbuzi huo, inayo uwezo mkubwa wa kupanuka na kukua kwa haraka na isipopagiliwa vizuri kutokea mwanzo inaweza kuishia ikipanuka kwa ujenzi holela.
“Chukulia mfano wa Jiji la Dar es Salaam Mheshimiwa Waziri.
Mamilioni ya watu wanaishi katika jiji hili lakini asilimia 70 ya mji
huu haikupimwa na imejengwa holela tu. Ni asilimia 30 ya Dar es Salaam
iliyopimwa. Hatuwezi kuiruhusu miji mingine, hasa ya kimkakati, kupanua na kukua kwa namna hii.”
Baada ya kumsikiliza Rais Kikwete, Waziri Weixin alisema kuwa ameelewa changamoto zinazoikabili Tanzania na kuwa Wizara yake itatuma wataalam wake kuja Tanzania kufanya tathmini katika maeneo muhimu kwa kushirikiana na wataalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo Waziri wake, Mheshimiwa Anna Tibaijuka alihudhuria mazungumzo hayo.
Rais
Kikwete na Waziri Weixin pia walizungumzia hali ya uhusiano kati ya
nchi na wananchi wa nchi hizo mbili ambao utafikisha miaka 50, Mei,
mwaka huu, 2014, kufuatia kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya
nchi hizo mwaka 1964.
“Tanzania
imenufaika sana na uhusiano huu katika miaka 50 ilitopita. China
imeisaidia sana katika miaka 50 hiyo. Tunahitaji kuuendeleza uhusiano
huu na bado tunahitaji kuendelea kuungwa mkono na China kwa sababu
pamoja na yote, Tanzania bado ni nchi inayoendelea.”
Imetolewa na; Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu,
DAR ES SALAAM
13 January,2014
Imetolewa na; Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu,
DAR ES SALAAM
13 January,2014