Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo amekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiache kumsakama Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kwa sababu tu ya kutaka kutimiza ndoto yake.
Ndesamburo
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, alisema kama ni
kuonyesha nia wapo wanachama wengine wa CCM wamefanya hivyo bila
kusakamwa.
Lowassa
anatajwa kuwa miongoni mwa wanaousaka urais mwaka 2015, na harakati
zake hizo zinaonekana kuwakera baadhi ya viongozi wa CCM ambao wameanza
kumwandama kwa maneno.
Tayari
CCM kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake, Philip Mangula na Katibu wa
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye wamekaririwa wakisema walioanza kampeni
mapema watashughulikiwa.
Hata
hivyo hakuna mahali popote ambapo Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa
Monduli amewahi kutangaza nia ya kuusaka urais isipokuwa amesema ana
ndoto ambayo iko mbioni kutimia.
Akitoa
salamu zake za mwaka mpya wa 2014 jana, Ndesamburo alisema si haki kila
matamko ya viongozi wa CCM kumlenga Lowassa pekee wakati wapo wanachama
wengine ndani ya CCM.
“Wanaotangaza nia mbona wako wengi sana huko CCM na wala siyo Lowassa peke yake,” alisema na kuongeza;
“Hao
wanaomnyooshea kidole Lowassa hawa wengine hawawaoni?” alihoji
Ndesamburo na kuwataka viongozi wa CCM kuacha unafiki na kuendesha mambo
kwa “double standard” (ubaguzi).
Ndesamburo
alisema ukimwondoa Lowassa, wapo wanachama wengine wa CCM wanaoshiriki
kwenye harambee kanisani na misikitini, lakini hilo haliwagusi viongozi
wa CCM isipokuwa Lowassa tu.
Credit: Gazeti la Mwananchi.