Mwenyekiti
wa mtaa wa pangani kata ya Makorongoni mjini Iringa Salum Kibaya
akiutazama mwili wa mtoto Raymond Ben Mangungu (2) aliyeuwawa kwa
kukabwa shingo na baba wa kambo wakati wa ugomvi wa kimapenzi kati ya
mwanaume huyo na mama wa mtoto huyo usiku wa leo.
Askari polisi akitazama mwili wa mtoto huyo.
Hali ilivyokutwa ndani ya chumba hicho baada ya tukio.
Wananchi wa Makorongini wakimtazama mwanamke huyo wakati akihojiwa na kaka wa mtuhumiwa wa mauwaji hayo.
Mama
wa mtoto Raymond katikati akimsimulia shemeji yake jinsi ambavyo
mpenzi wake alivyoua mtoto ,kushoto ni mama mzazi wa mwanamke huyo.
Huyu ndie mzazi wa mtoto aliyeuwawa Bi Kudra Kahemela (23)Wanawake wa mtaa wa Pangani Iringa wakiuhifadhi mwili wa mtoto Raymond leo.
KATIKA
hali isiyo ya kawaida mwanaume mmoja mkazi wa mtaa wa Pangani kata
ya Makorongoni katika Manispaa ya Iringa Hamis Said maarufu kwa jina
la Mwarabu amemuua kinyama mtoto Raymond Ben Mangungu (2) kutoka na
ugomvi wa kimapenzi kati yake na mama wa mtoto huyo ambae kwake ni
mpenzi wake .
Imedaiwa
kuwa mtuhumiwa huyo wa mauwaji ya mtoto huyo alikuwa amelewa
pombe kupita kiasi na si mara ya kwanza kulewa kiasi hicho na
kutishia kufanya mauwaji dhidi ya mtoto huyo wa kambo kwa kile
alichokuwa akidai kuwa ni fedhea kwake kuishi na mwanamke ambae ana
watoto wawili ambao si damu yake.
Wakizungumzia
juu ya tukio hilo mashuhuda wa tukio hilo kwa sharti la kutotaja
majina yao walisema kuwa imekuwa ni kawaida kwa Mwarabu kumpiga
mwanamke huyo na familia yake kwa madai kuwa hataki kuwaona watoto
hao wakiendelea kuishi katika nyumba hiyo ambayo ameipanga yeye .
"
Huyu bwana Mwarabu alikuwa akifanya kazi ya kuuza korosho mitaani na
akirudi usiku amekuwa mkali kwa mwanamke huyo ambae alikuwa akidai
kuwa bado amekuwa na mahusiano na baba wa watoto hao wawili
.....hata hivyo sisi kama majirani tumekuwa tukishindwa kuwaamua
kutokana na mwanaume kuwa na tabia ya kulewa pombe kupita kiasi na
hata tukio hili tulijua ni kawaida yao "
Mtoto
Tinito Mangungu (6) ambae ni kaka na marehemu alisema kuwa baba
yao huyo mdogo alifika usiku na kuwataka wote kuamka kitandani na
kuwa hakuna mtu atakayelala katika chumba hicho kama si damu yake.
"Baba
mdogo (Mwarabu) alirudi usiku akiwa amelewa na kusema hakuna mtu
kulala kitandani na kuanza kumpiga mama kwa meza na viti huku sisi
tukilia kumtaka asimpige mama yetu....baada ya hapo alimchukua mdogo
wangu na kuanza kumkaba shingo na kumwacha kitandani akiwa amelala
bila kuamka hadi sasa mama anasema amekufa"
Akielezea
juu ya mkasa huo uliosababisha mauwaji ya mtoto Raymond mama mzazi
wa mtoto huyo Bi Kudra Kahemela (23) alisema kuwa kwa upande wake
baada ya kutishiwa kuuwawa kwa kipigo alifanikiwa kukimbia katika
chumba hicho na kwenda kujificha nje na baada ya muda mwanaume huyo
alianza kutapika na pale alipoingia kutana kumsaidia ndipo alipopigwa
na kuamua kukimbia kwenda kulala nje ya nyumba hiyo kwa kujiegesha
katika nguzo ya umeme iliyopo nyumba ya pili karibu na nyumba ya
shekhe wa mkoa Juma Alli Tagalile
Alisema
kuwa asubuhi aliingia katika chumba hicho baada ya mwanaume huyo
kutoka kwenda katika kilabu cha pombe za kienyeji cha Tulivu
kuendelea kunywa pombe na kumkuta mtoto huyo akiwa amelala bila
kutikisika .
"
Mimi nilijua kama mtoto amelala tu ama amezimia ila baada ya kuwaita
watu wazima akiwemo mama yangu mzazi ndipo nilipobaini kuwa mtoto
wangu Ray amefariki dunia na ndipo nilipomfuata na kumweleza juu ya
tukio hilo ila bado aliendelea kunywa pombe na kudai kuwa mtoto
huyo amezimia kwa kelele za usiku ."
Alisema
baada ya hapo mwanaume huyo alikimbia hadi Ilala kwa wakwe zake na
kuomba msamaha na kusuluhishwa ugomvi wao ila wakati mtengo wa
kukamatwa ukiwekwa ndipo alipokimbia kusiko julikana.
Mwandishi
wa habari hizi alishuhudia mtoto huyo akiwa amekufa katika kitanda
cha wazazi wake huku chini ya chumba hicho thamani mbali mbali
pamoja na vyombo vikiwa vimevunjika kutokana na ugomvi huo .
Mwenyekiti
wa serikali ya mtaa huo wa Pangani kata ya Makorongini Bw Salum
Kibaya amethibitisha juu ya kifo cha mtoto huyo na kuwa baada ya
tukio hilo ambalo lilitokea usiku wa kuamkia leo jumamosi Desemba 14
mwaka huu alilazimika kwenda kituo cha polisi cha stendi kuu ya
mabasi yaendeyo mikoani na kuwajulisha juu ya tukio hilo na kufika
eneo la tukio .
Bw
Kibaya alithibitisha pia kuwa ugomvi kati ya wapenzi hao si wa
kwanza kutokea japo kwa maelezo ya mwanamke huyo alikuwa mbioni
kuolewa na mwanaume huyo na hivyo kuwa na wanaume wawili akiwemo mzazi
mwenzake ambae kwa sasa anaishi eneo la Don Bosco mjini hapa.
Mwili
wa mtoto huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa
Iringa huku jeshi la polisi likiwahoji mama wa mtoto huyo ,kama wa
mtuhumiwa wa mauwaji hayo ambae ni mkazi wa Mlandizi Kibaha Jijini Dar
es Salaam na mama mzazi wa mtoto aliyepoteza maisha.
CHANZO NI FRANCIS GODWIN