Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Willbroad Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Willbroad Slaa, akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kasulu Vijijini alisema kama gongo itatengenezwa kwa mitambo maalum itaondoa mianya ya rushwa kwa polisi ambao wamekuwa wakiwakamata wanaotengeneza kwa kificho na kuwafanya vitega uchumi vyao.
"Gongo sasa hivi ni haramu sababu inatengenezwa kwa kificho katika mazingira machafu, tukishika dola tutataka SIDO itengeneze mitambo ya kutengeneza gongo ili iwe katika hali ya usafi," alisema.
Mitambo hiyo itakayotengenezwa na SIDO itakapouzwa itaiingizia mapato serikali pia wauzaji wa gongo watafanya biashara hiyo kwa amani tofauti na sasa ambapo wanaifanya kwa kificho na wakikamatwa fedha zote wananufaika polisi.
Dk. Slaa alisema hata suala la kukamata watu wanaotengeneza silaha linapaswa kuangaliwa upya kwani wanaokamatwa wakifanya kazi hiyo wangekuwa wanashikiliwa kwa muda na baadaye wanapelekwa katika kiwanda cha serikali cha kutengenezea silaha ili watuhumiwa hao wapeleke ujuzi huo huko badala ya kuwafunga jela.
Dk. Slaa alisema matatizo yote yanatokana na wasomi kutofikiri namna ya kuisogea nchi mbele kimaendeleo.
"Nchi hii imelala, imechoka sababu waliopewa madaraka wamelala, wamejisahau hawatambui kuwa wamepewa nafasi hizo ili kuwatumikia wananchi," alisema.
CHANZO: NIPASHE