Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba amesema kuwa anatafakari iwapo awanie urais
katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, kutokana na kuwapo kwa watu wengi hasa
ndani ya CCM, wanaomtaka kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
Makamba ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM alisema: “Kwanza
ni kweli kwamba kuna ushawishi kuhusu suala hilo kutoka kwa vijana
walioko nje na ndani ya chama, wanataaluma, baadhi ya wazee na watu
wengine iwe kwa makundi au mtu mmoja mmoja wamekuwa wakinishawishi
kugombea kwa muda sasa.”
Aliongeza: “Mwanzoni sikuona uzito
sana, yaani sikuzingatia sana, lakini kwa kadiri siku zinavyokwenda ni
kwamba ushawishi umekuwa mkubwa na hivyo niseme ni jambo ambalo sasa
ninalitafakari kwa kina”.
Alisema ikiwa ataamua kuwania urais,
atafanya hivyo wakati mwafaka kwa kuzingatia utaratibu utakaowekwa na
chama hicho, lakini akasema kwa sasa si wakati wake. Makamba alikuwa
akijibu hoja za gazeti hili lililotaka ufafanuzi wake kutokana na kuwapo
kwa taarifa kwamba ameanza harakati za kuusaka urais katika Uchaguzi
Mkuu wa 2015.
Gazeti hili lilidokezwa kuwa hatua yake
hiyo imemwingiza katika mvutano usio rasmi na wanasiasa ambao tayari
wameonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini,
wakiwamo wale wa kambi ya urais aliyokuwa akidaiwa kuwa mmoja wao.
Awali iliaminika kuwa Makamba alikuwa
katika kambi ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, lakini wachambuzi
wa masuala ya kisisa wanasema ‘katika siku za karibuni mwenendo wake
unaashiria kwamba si mmoja wa wanaomuunga mkono kiongozi huyo, bali ni
mtu mwenye mipango yake binafsi ya kisiasa”.
Habari ambazo Mwananchi imezipata
zinasema mwenendo wa Makamba umewakasirisha baadhi ya wanasiasa hususan
wanaomuunga mkono Lowassa ambao mara kadhaa wamesikika hadharani
wakimlalamikia kwamba ni msaliti.
Hata hivyo, Makamba katika maelezo yake
anasema hajawahi kuwa katika kundi lolote la kumuunga mkono mtu yeyote
kwani yeye haamini katika makundi. “Ninaamini katika kundi moja, nalo ni
CCM,” alisema.
Aliongeza: “Kwa
hiyo mtu yoyote akinikasirikia kwa sababu zozote zile za kisiasa
nitamshangaa maana sijawahi mahali popote na kwa namna yoyote
kujitanabaisha kwamba mimi nipo kwenye kundi fulani, au kundi la mtu
yeyote.”
Sababu za mashaka
Miongoni mwa nyedo zinazotiliwa shaka
za mwanasiasa huyo ni hatua yake ya kushiriki katika Mkutano Mkuu
Maalumu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) uliofanyika Zanzibar ambako
pamoja na mambo mengine aligawa simu zaidi ya 100 aina ya Samsung Galaxy
kwa wajumbe wa mkutano huo.
Imethibitika kwamba mpango huo ulikuwa
ni wake binafsi na haukuwashirikisha waliokuwa wakiamini kwamba wako
naye katika harakati za kumuunga mkono Lowassa.
Tukio jingine ni lile la vijana
waliojitambulisha kuwa viongozi wa vyuo vikuu nchini kutangaza katika
mkutano wao mjini Morogoro kwamba watamwomba Makamba awanie urais katika
Uchaguzi Mkuu ujao, kutokana na kile walichodai kwamba ni matokeo ya
kura walizopiga baina ya kiongozi huyo na viongozi wengine vijana; John
Mnyika na Zitto Kabwe wa Chadema.
Wapinzani wake wanaamini kwamba tamko
la vijana hao zilikuwa mbinu binafsi za Makamba kutaka kuonyesha kwamba
naye anakubalika na pengine maandalizi ya kujiengua rasmi kutoka katika
kambi yake ya awali.
Wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya
miaka 14 ya kifo cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Makamba alikuwa
Butiama mkoani Mara ambako mbali na kushiriki Ibada ya kumwombea Baba wa
Taifa, pia alikuwa mgeni rasmi katika kongamano la kumuenzi kiongozi
huyo.
Kuhusu baadhi ya makada wenzake kukasirishwa na mwenendo wake kisiasa, Makamba alisema: “Hata
mimi nimesikia kama wewe unavyosema umesikia, inawezekana
wanakasirishwa na mvumo maana ndani ya chama chetu watu wanazungumza
sana, tena hadharani kwa hiyo katika mazingira hayo taarifa zinaweza
kumfikia yeyote kama zilivyokufikia wewe”.
Alitetea hatua yake ya kugawa simu
kwenye mkutano wa UVCCM akisema alikuwa akitimiza ahadi aliyoitoa wakati
wa semina ya vijana hao Februari mwaka huu mjini Dodoma, pale
walipomuomba kuwasaidia ili waweze kutekeleza matakwa ya ushauri wake wa
kukitetea CCM katika mitandao ya kijamii.
“Mimi kwa
nafasi yangu nikiwa Naibu Waziri wa masuala ya teknolojia, nikiombwa
kusaidia lolote katika eneo langu ndani ya chama sioni tatizo ilimradi
niwe na uwezo nalo, kwa hiyo nilitimiza ahadi yangu tena kwa uwazi
sikufanya kwa kificho,”alisisitiza.
Makamba ni mwanasiasa wa tatu kijana
kutajwa kuwa huenda akawania urais, wengine wakiwa ni Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja.
Wengine ambao wameishaonyesha nia ya
kuutaka urais ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta
na Lowassa.
Vita ya urais imekuwa ikikiumiza CCM,
ambapo Makamu Mwenyekiti wake (Tanzania Bara), Philip Mangula aliwahi
kukaririwa akiwaonya makada wa chama hicho ambao wameanza kupiga mbio za
kuusaka uongozi huo kuwa hawatavumiliwa, kwani harakati hizo zimekuwa
kichocheo cha mgawanyiko ndani ya chama.
Mwananchi