MTOTO wa kike
mwenye umri wa miaka mitatu, Maryment Ibrahim ambaye anaishi Tandale
jijini Dar es Salaam, hivi karibuni alipatwa na masahibu makubwa baada
ya kutekwa nyara na kutoroshwa hadi Gairo mkoani Morogoro huku mtekaji
akidaiwa kutaka apewe shilingi milioni 6 ili amuachie.
Tukio
hilo la kusikitisha lilitokea Oktoba 16 mwaka huu baada ya kijana
mmoja, anayefanya biashara ya kuuza chipsi anayejulikana kwa jina la
Issa Ramadhani, kudaiwa kumchukua mtoto huyo aliyekuwa akicheza nyumbani
kwao na kutoweka naye kabla ya wazazi wake kubaini na kwenda kutoa
taarifa kituo cha Polisi Kijitonyama ‘Mabatini’.
Awali, ilidaiwa
Ramadhan alikuwa na tabia ya kuwachukua watoto wadogo wa mtaani hapo na
kuondoka nao na kuwarudisha baadaye, kitu kilichowafanya wazazi wa
mtoto huyo kutokuwa na wasiwasi.
Wakizungumza
na mwandishi wetu, wazazi wa mtoto huyo walisema waliamua kutoa taarifa
polisi na kufunguliwa jalada nambari KJM/RB/8994/13 baada ya kupashwa
kuwa mtekaji ambaye alishaacha kazi yake ya kukaanga chipsi, aliondoka
muda mrefu na binti yao na hakukuwa na dalili za kurejea.
Baada ya
kuhangaika kwa muda mrefu, wazazi hao pamoja na majirani walifanya
uchunguzi wa chinichini na kufanikiwa kupata namba ya simu ya mtekaji
huyo, lakini walifanikiwa kubadilishana naye ujumbe mfupi wa simu kwani
hakuwa akipokea simu yake ya kiganjani.
Inadaiwa kuwa katika mawasiliano hayo, mtekaji alikataa katakata ombi la kumtaka amrudishe
mtoto wao na
kutaka apewe kiasi cha shilingi milioni 6 ili kutekeleza jambo hilo
ingawa baadaye ilibainika jamaa huyo alikuwa Gairo mkoani Morogoro.
Wazazi hao
walisema kuwa Oktoba 19 mwaka huu mmoja wa majirani walioguswa na tukio
hilo aliyejitambulisha kwa jina la Justin Henry alijitolea kusafiri
mpaka Gairo kumsaka mtoto na mtekaji wake jambo ambalo lilifanikiwa kwa
kumpata mtoto akiwa mzima wa afya japokuwa mtekaji alishtukia na
kukimbia.