VITUO vya daladala vya Ubungo na Mwenge vinahamishwa kupisha Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart), ambao miundombinu yake inaendelea kujengwa.
Kituo
cha Ubungo kitahamishiwa nyuma ya jengo la Mawasiliano lililopo
Barabara ya Sam Nujoma, vivyo hivyo kituo cha Mwenge, kitatumika kwa
ajili ya kushusha abiria pekee.
Ofisa
Habari wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera amesema, magari ya
Mwenge, yatakuwa na uamuzi wa ama kuishia kwenye stendi ya Makumbusho
;au kwenda hadi kituo hicho kitakachohudumia magari ya Ubungo kilichoko
Mawasiliano.
Kwa mujibu wa Mhowera, wakati wowote kuanzia sasa vituo hivyo, vitabomolewa kupisha mradi huo.
Hata
hivyo, hakuelezea kwa undani juu ya maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho
kipya. Alisema hayo alipozungumza na mwandishi wa habari hizi, kuhusu
hatua zinazochukuliwa na manispaa, kuwezesha wafanyabiashara ndogo
kupata maeneo ya kuendesha shughuli zao.
Alisema
baada ya kituo cha Ubungo kuhamishiwa katika eneo hilo jipya,
hakutakuwa na mfanyabiashara atakayeruhusiwa kuuza bidhaa zozote kama
ilivyo sasa.
Alisema
kuhamishwa kwa vituo hivyo, kutatoa nafasi kwa wafanyabiashara kwenda
katika maeneo waliyopangiwa kwa kuwa hakutakuwa na nafasi, kwani yote
yatatumika kwa ajili ya barabara.
“ Kwa hiyo ni bora wakaanza kujiondosha wenyewe mapema kabla hatua ya kuondolewa na ujenzi kuwafikia,” alisema.
Kwa
mujibu wa ofisa habari huyo, yapo maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kazi
hiyo katika masoko mbalimbali likiwemo laKijitonyama.
-Habari leo
-Habari leo