Home » » SERIKALI KUFANYIA MAREKEBISHO SHERIA YA NDOA ILI KUMUOKOA WATOTO WA KIKE WANA OLEO KATIKA UMRI MDOGO..

SERIKALI KUFANYIA MAREKEBISHO SHERIA YA NDOA ILI KUMUOKOA WATOTO WA KIKE WANA OLEO KATIKA UMRI MDOGO..

SERIKALI imesema inaangalia uwezekano wa kubadili sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ambayo inaruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 15 badala yake iruhusu umri wa kuolewa uanzie miaka 18.
Aidha imeeleza kuwa ndoa za utotoni kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikirudisha nyuma maendeleo ya watoto wa kike, kutokana na wengi wao kuachishwa shule na kuozeshwa.
Hayo yameelezwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe wakati akizungumza katika majadiliano ya ngazi ya juu kuhusiana na ndoa za utotoni, ambapo jana ilikuwa ni Siku ya Mtoto wa Kike Duniani.
Waziri Chikawe alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya sasa mtoto wa miaka 15 anaruhusiwa kuolewa kwa idhini ya wazazi wake, jambo ambalo amewataka wadau wote kushirikiana kuhakikisha sheria itambue umri wa ndoa uwe ni miaka 18 na si vinginevyo. Hata hivyo, Waziri Chikawe alisema suala la kubadili sheria hiyo linatarajiwa kuchukua zaidi ya miaka mitatu, ili kukomesha kabisa ndoa za utotoni.
"Serikali inatambua uwepo wa ndoa za utotoni na hili ni tatizo kubwa sana, hivyo mbali na kurekebisha sheria lakini pia tunahitaji kuwapa wananchi wetu elimu zaidi kuhusiana na ndoa za utotoni ili hata wao wajue madhara yake," alisema Waziri Chikawe.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Valerie Msoka alisema suala la ndoa za utotoni bado ni changamoto kwa nchi zote za Afrika, ambapo Tanzania inaonekana kuwa ni ya 20, jambo ambalo alisema ni lazima serikali iungane na taasisi mbalimbali kulitetea jambo hilo.
"Kikubwa ni elimu iendelee kutolewa kwa wananchi wote, pia tunafarijika kuona kuwa sasa serikali itaenda kubadilisha sheria ya ndoa kutoka miaka 14 kwenda miaka 18, japo napo ni bado ingekuwa hata miaka 21 lakini kwa kuanza si mbaya" alisema Msoka.
-Habari Leo
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger