RAIS Jakaya Kikwete amewatoa hofu Watanzania kwamba kuwaruhusu wawekezaji wa nje kufanya utafiti wa mafuta na gesi nchini, kuna hasara kubwa itakayolikumba taifa. Pia amewataka kupuuzia dhana kwamba kuwaruhusu wawekezaji hao kunaweza kusababisha wahamishe rasilimali za gesi na mafuta zitakazogunduliwa kunufaisha mataaifa ya nje.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo, Dar es Salaam jana kabla ya kuzindua awamu ya nne ya ugawaji vitalu baharini katika kina kirefu Kaskazini mwa Ziwa Tanganyika.
“Kumekuwa na maneno mengi kuwa mfumo huu wa sasa wakutoa leseni za utafutaji wa mafuta na gesi kwa wawekezaji wa nje, kuwa hakuwanufaishi Watanzania.
Alisema sheria, mfumo na mikataba iliyowekwa haiwezi kuruhusu mianya hiyo ya kupata hasara na kwamba asilimia 75 ya faida itakayopatikana baada ya wawekezaji kurudisha gharama zao za utafiti, itakuwa ni ya taifa na asilimia 25 ndiyo itakayokuwa stahili yao.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete wapo baadhi ya watu wanaoeneza maneno potofu, kwamba Watanzania watapata hasara kutokana na uwekezaji huo, na kufafanua kwamba wanaosema hivyo hawaujui ukweli.
"Sisi Watanzania hatupati hasara katika uwekezaji huu, tutapata faida kubwa na wanaojidanganya tutapata hasara hawana uelewa wa hili," alisisitiza Rais.
Kuhusu uwekezaji huo, Rais Kikwete alisema ili kufanya utafiti unatakiwa kuwa na fedha nyingi na kutolea mfano kuchimba kisima kimoja cha mafuta hugharimu dola za Marekani milioni 100.
"Serikali hatutoi mchango wowote katika utafiti huo, na teknolojia inayotumika ni kubwa ambayo sisi hatuna uwezo. Tunasubiri wawekeze kisha tuje kugawana faida na asilimia 75 au 65 ni yetu. Hasara iko wapi katika mfumo huo," alihoji Rais.