RAIS Jakaya Kikwete amewataka wanaume kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata tohara, kama moja ya njia za kukabiliana na Ukimwi unaoendelea kuua watu wengi.
Akisalimia wananchi katika Kijiji cha Kipengele kilichoko Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe, ambako anaendelea na ziara yake kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo, aliwapongeza wanaume ambao hadi sasa wamejitokeza kupata tohara kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Aliwaambia wananchi waliohudhuria mkutano wake wa hadhara kuwa kwa mujibu wa wataalamu, majaribio ya tohara ambayo yamekuwa yanaendelea katika Mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe, yameonyesha mafanikio hata kama mikoa hiyo ndiyo inaendelea kuongoza nchini kwa maambukizi ya ugonjwa huo.
“Miaka michache iliyopita, tulianzisha kampeni ya tohara kwa wanaume wa Mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe kwa majaribio na kwa ushauri wa madaktari. Sasa wataalamu wanatuambia kuwa kampeni hiyo imekuwa ya mafanikio makubwa sana.
“Naambiwa kuwa mwitikio wa kampeni hii umekuwa mzuri sana. Endeleeni. Nawapongeza wale ambao wameshiriki shughuli hiyo hadi sasa na kuwashauri wale ambao bado nao wafikirie namna ya kujiunga kwenye kampeni hiyo. Kama wewe bado basi jitahidi ujiunge,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, alifafanua kuwa watu wasije kufirikia kuwa tohara pekee yake inatosha kuzuia maambukizi ya Ukimwi.
“Kufanya tohara hakuna maana kuwa mtu hawezi kupata Ukimwi. Tohara sio kinga wala tiba ya Ukimwi kwa sababu tiba na kinga za Ukimwi bado kupatikana.
“Wanachosema wataalamu, hata hivyo, ni kwamba mtu mwenye tohara anayo nafasi kubwa zaidi ya kuepukana kupata Ukimwi kuliko yule ambaye hana tohara na siyo kwa Ukimwi tu bali kwa magonjwa mengi ambayo yanaambukizwa kwa njia ya kufanya mapenzi,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete yuko katika ziara ya siku saba katika Mkoa wa Njombe na jana ameingia katika siku yake ya tatu kwa kutembelea Wilaya za Wanging’ombe na Makete.
-Mtanzania