Mwajuma Haji wakati wa uhai wake. |
INAUMA SANA! Yule mtoto ambaye Amani liliripoti kuwa ndugu wanataka auawe wiki iliyopita, Mwajuma Haji (16), amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar.
Mama mzazi wa Mwajuma akimhudumia mwanaye wakati wa uhai wake. |
Akizungumza na mwandishi wetu kwenye mazishi ya mtoto huyo kijijini kwao Kimange, Wilaya ya Bagamoyo, Tatu alisema mwanaye alizidiwa kwa siku tatu mfululizo huku akiwa anapumulia mashine kabla mauti hayajamkuta. Alisema madaktari walijitahidi kwa hali na mali kuokoa maisha yake lakini ilishindikana kwani alikuwa akipumua kwa shida.
“Mwanangu ameteseka sana dakika za mwisho kwani kwa siku tatu mfulululizo alikuwa akipumulia gesi tu mpaka Mungu alipomchukua,” alisema mama huyo. Katika mazishi ya mtoto huyo, waliokuwa karibu na mama Mwajuma ni majirani zake baada ya ndugu kuingia mitini.
Majirani wa karibu na mama Mwajuma waliliambia Amani kuwa wanasikitishwa na tabia za ndugu zake waliosusia msiba huo na kudai ndiyo tabia yao kwani kipindi Mwajuma alipokuwa hai walikuwa hawamjali hata walipomkuta akinyeshewa mvua hawakumuingiza ndani hadi mama yake alipofika.
“Tabia za ndugu wa mama Mwajuma hazijaanza leo kwani walikuwa wakimtenga sana mtoto huyo kwa kuwa hata walipomkuta ananyeshewa na mvua walikuwa wakimuacha hadi mama yake arudi,” alisema jirani mmoja ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.