Masogange anakuja Bongo baada ya kumaliza kulipa deni lote la randi 30,000 (shilingi milioni 4.8) alizoamriwa kulipa na Mahakama Kuu ya Gauteng iliyopo Kempton Park jijini Johannesburg nchini humo baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kuingiza kemikali haramu, Julai 5, mwaka huu.
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika, Masogange anarejea na Melisa Edward ambaye alikamatwa naye lakini mahakama ikamwona hana hatia.
SIRI NZITO
Ujio wa Masogange bado una siri nzito kwani licha ya mahakama hiyo kumtia hatiani kwa faini au kifungo cha miezi thelathini jela, lakini bado serikali ya Tanzania inahaha kutaka kujua mzigo aliodakwa nao alitumwa na nani!
“Masogange ameahidi kutowataja watu waliompa mzigo akidai kuwa itaendelea kuwa siri yake mpaka anakufa,” kilipasha chanzo chetu.
WATOTO WA VIGOGO
Watoto wa vigogo ndiyo wamekuwa wakitajwa zaidi kuhusika na kumtuma Masogange ingawa hakuna jina la moja kwa moja la mtoto yeyote wa kigogo lililowahi kutajwa.
ANAYEMJUA MWAKYEMBE
Mpaka sasa, Serikali ya Tanzania kupitia kwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison George Mwakyembe iliwahi kumtaja kijana aitwaye Mangunga ambaye ndiye anadaiwa kuwa na Masogange ndani ya ndege kwenda Afrika Kusini.
Mwakyembe aliamuru kijana huyo asakwe na kukamatwa ili kujibu mashitaka ya kusafirisha madawa ya kulevya aina ya Methamphetamine kwa Tanzania huku Afrika Kusini ikisema unga huo ni ephedrine ambao si wa kulevywa bali ni kemikali haramu.
KAMATI YA MAPOKEZI YAMWANDALIA PATI YA MAMILIONI
Habari za kifukunyuku zinadai kuwa, jijini Dar baadhi ya mastaa wameunda kamati ya mapokezi ya Masogange, Jacqueline Wolper Massawe akiwa mwenyekiti wake, katibu na wajumbe hawakupatikana majina.
KAZI YA KAMATI
Kazi ya kamati hiyo inadaiwa ni kukusanya mamilioni kutoka kwa mapedeshee wa mjini ili kuwezesha kufanyika kwa pati ya nguvu ya kumshukuru Mungu kwa kumsaidia staa huyo kutoka jela na kurudi Bongo.
“Kamati iko chini ya uenyekiti wa Wolper, si unajua huyu dada hata hivi karibuni alimfanyia birthday Masogange japo mwenyewe hakuwepo?
“Sherehe itaandaliwa kwenye ukumbi mmoja uliopo ufukweni mwa Bahari ya Hindi lakini kwa sasa sitautaja ili kuepuka wazamiaji,” kilisema chanzo chetu.
NZOWA: HIYO PATI ITAFANYIKIA WAPI, SINZA KWA DADA’KE AU?
Kufuatia kuwepo kwa madai kwamba, Masogange akitua tu Bongo atadakwa na Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, juzi Amani lilimsaka kamanda wa kikosi hicho, Godfrey Nzowa na kumuuliza kuhusu madai hayo.
Amani: Afande, naomba unisaidie mawili matatu. Yule msanii Masogange aliyekamatwa na madawa ya kulevya na kuhukumiwa Afrika Kusini anarejea nchini kesho Jumatano (jana) Je, ninyi mna mpango wowote wa kumkamata akitua?
Nzowa: Sisi hatuna shida naye tena. Alishahukumiwa kule, sasa tumkamate huku kwa sheria gani?
Amani: Basi kuna habari kwamba mmepanga kumkamata maana tumeambiwa na chanzo chetu kuwa atafanyiwa pati ya kumshukuru Mungu kwa kumtoa katika mazito.
Nzowa: Hiyo pati ataifanyia wapi, Sinza kwa dada’ke au?
Amani: Bado hawajaweka wazi.
Nzowa: Sisi hatuna shida naye.
WOLPER ASAKWA KUULIZWA
Juzi asubuhi, Amani lilimtafuta Wolper kwa njia ya simu yake ya mkononi na kumuuliza ukweli wa kuwepo kwa kamati ya sherehe ya mapokezi ya Masogange ambapo alijibu:
“Nipo shooting (narekodi) Arusha, nitawatafuta baadaye kuhusu hilo suala kama lipo au halipo.”
MASOGANGE NAYE
Juzi Jumanne, Amani lilimpigia simu Masogange akiwa Afrika Kusini na kumuuliza kuhusu ujio wake wa jana.
Masogange: Ni kweli narudi huko (Bongo) Jumatano, mipango yote ya safari tayari, namshukuru Mungu kwa yote.
WENGINE WANASOTA!
Wakati Masogange akiwa ameponea tundu la sindano, mrembo mwingine wa Bongo Fleva, Sandra Khan ‘Binti Kiziwi’ anateseka gerezani huko China alipofungwa kwa miaka mitatu kwa msala wa madawa ya kulevywa wakati Saada Kilongo yuko mahabusu Bongo kwa kesi ya aina hiyohiyo.