Home » » Kapten Komba ajitoa mhanga:...Adai kuwa Lowassa ndo Rais mteule wa watanzania- 2015 baada ya Kikwete

Kapten Komba ajitoa mhanga:...Adai kuwa Lowassa ndo Rais mteule wa watanzania- 2015 baada ya Kikwete


Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kapteni Mstaafu, John Komba amevunja ukimya na kutamka wazi kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ndiye chaguo lake na atakuwa Rais ajaye uchaguzi wa 2015. 
 
Komba anakuwa mtu wa pili kumtaja Lowassa hadharani kuwa anafaa kuwa rais 2015.
 
Itakumbukwa Mbunge wa Viti Maalumu, Beatrice Shelukindo (CCM) naye alivunja ukimya baada ya kutangaza kumuunga mkono Lowassa kumrithi Rais Kikwete.
 
Shelukindo alitoa kauli hiyo wakati akiwasalimia wakazi wa Monduli baada ya kukaribishwa kuchangia ujenzi wa Hosteli ya KKKT, kwenye sherehe za kukaribisha Mwaka Mpya zilizofanyika nyumbani kwa Lowassa na kuhudhuriwa na makada kadhaa wa CCM.
 
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu jana, Komba ambaye ni Kiongozi wa Kundi la Uhamasishaji cha CCM Tanzania One Theatre (TOT Plus), alisema mtazamo wake kwa mtu anayefaa kumrithi Rais Jakaya Kikwete ni Lowassa.
 
Komba aliyeingia kwenye siasa kutokana na msukumo wa mama yake aliyekuwa msaidizi wa Bibi Titi Mohamed, alisema anazo sababu kuu tano za kumkubali Lowassa kuwa Rais na atasimama popote kumtetea.
 
“Nakuambia Lowassa ndo  anafaa kuwa Rais  na nina sababu zangu tano za kusema hivyo,” alisema Komba na kuhoji:
 
“Wewe unakwenda kwenye harambee, nani leo hii anaweza kusaidia kuchangia fedha nyingi na zote hizo ni kwa maendeleo yanayokusudiwa kama siyo Lowassa?” alisema Komba ambaye ni mahiri katika kuinadi CCM, katika kampeni mbalimbali za udiwani, ubunge na urais.

Juu ya kuwa atakuwa katika wakati mgumu endapo anayempigia debe hatokuwa Lowassa, Komba alisema:
 
“Mimi nimesema namkubali Lowassa, lakini kama akiteuliwa mwingine, mimi nitakuwa naye...nitamwimbia hadi mwisho. Kazi yangu si unaijua, nitampigia debe kwa kuwa si mtu wa mtu mmoja, ni uteuzi wa wanaCCM ule si wa Komba.” .
 
Mbali na kumnadi Lowassa, Komba alisifu uimara wa chama chake kuwa kinaimarika siku hadi siku na ndicho kinachotoa viongozi wa kweli na hata wananchi wanakikubali.
 
Akizungumzia suala la rushwa ndani ya CCM, Komba ambaye pia ni Mbunge wa Mbinga, alisema kama chama kuna watu wa aina nyingi, kuna wasafi, kuna wachafu lakini wote wako kwenye mstari mmoja.

 Alisema kuwa vita ya rushwa ndani ya CCM itamalizika endapo kila kiongozi atasimamia  haki na maadili ya uongozi na pia kutambua wajibu wake ndani ya chama.

-Mwananchi

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger