MWANAFUNZI wa darasa la sita, Ismail Godfrey (13) anayesoma katika Shule ya Msingi Maendeleo Sinuka iliyopo mkoani Kigoma amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kudai kutandikwa viboko na Mwalimu Muige Joseph na kupooza miguu.
Mtoto Ismail Godfrey akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar.
“Awali sikuwa na matatizo yoyote ya kiafya hususan katika viungo vya mwili, isipokuwa haya yalinipata baada ya kuchapwa fimbo na mwalimu wangu ndipo nikapooza ghafla.
Miguu ya mtoto Ismail iliyopooza.
“Hapo hapo nikahisi viungo vyote vya mwili vimepoa na miguu ikapata ganzi, nikaanguka chini baada ya kukosa nguvu,” alisema Ismail.
Kutokana na tukio hilo baba wa mtoto huyo, Godfrey Lucas aliitwa na baada ya kuona Ismail yupo katika hali hiyo ya kupooza miguu aliamua kumpeleka katika Hospitali ya Mkoa, Maweni, kupatiwa matibabu, huku akifanya juhudi za kumtafuta mtuhumiwa ambaye alikuwa amekimbia makazi yake.
“Mtoto alianza kutokwa na vidonda miguuni ndipo nikaamua tuje hapa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na tukapokelewa na mtoto amelazwa wodi ya wagonjwa ya Kibasila,” alisema.
Hata hivyo, amesikitika kuachiwa mtuhumiwa kwa dhamana wakati mwanaye bado kalazwa na anakosa masomo kwa sababu yake.