Irene Malecela na mume wake, Sixmond Mdeka ‘Ras Six’ wakikata keki.
Irene Malecela na Sixmond Mdeka ‘Ras Six’ katika pozi.
Hamida Hassan na Gladness MallyaWANAMUZIKI wa kizazi kipya ambao ni wanandoa, Irene Malecela na mume wake, Sixmond Mdeka ‘Ras Six’, wamelieleza habari ya kusikitisha.
Wanamuziki hao ambao kwa sasa ni wazazi wa mtoto mmoja anayeitwa Jason, wamelieleza kuwa ulemavu walionao uliwafanya wakose wasimamizi kwenye ndoa yao.
Wawili hao mara baada ya kukosa wasimamizi kwa kila waliyekuwa wanakwenda kumwambia kuhusu suala hilo kukataa, walijitokeza Wazungu raia wa Italia ambao walikubali kuwasimamia.
Wakiongea kwa furaha nyumbani kwao Mbagala Maji-Matitu, wanandoa hao walisema wanafurahia sana maisha ya ndoa na wanawahimiza watu wengine wenye hali kama yao kutokata tamaa ya maisha na kama wana wapenzi wafunge ndoa kwani ni jambo lenye baraka na wasiogope vikwazo.
Walikutana vipi na kuanzisha uhusiano?
Six na Irene walikutana Kinondoni kwenye bendi inayoitwa Tunaweza ambapo walikuwa wakifahamiana kutokana na wote kuwa wasanii na kuanzisha rasmi uhusiano. Irene alikuwa miongoni mwa wanachama waanzilishi na Six akiwa meneja wa bendi hiyo.
Wawili hawa walianzisha uhusiano, yaani uchumba mwaka 2009 na 2011 mwishoni walifanikiwa kufunga ndoa yao na sherehe kufanyika kwenye Ukumbi wa Msasani Beach ambapo ilihudhuriwa na watu mbalimbali.
Kilichowanyong’onyesha kwenye ndoa
Wakati wakiandaa ndoa yao walijaribu kupita kwa kila mtu kutafuta wasimamizi lakini walikataliwa kwa kunyanyapaliwa huku kila mmoja akiwa na sababu yake. Walipokata tamaa, waliwaomba Wazungu ambao ni mke na mume ambao walikubali kuwasimamia ndoa yao.
“Ukweli tunawaheshimu sana Mr na Mrs Fundi waliokuwa hapa nchini kwani baada ya kuwaambia tu walikubali bila hata kuuliza swali la aina yoyote na walituunga mkono kwa hali na mali na kuifanya siku yetu kuwa ya kifahari,” alisema Sixmond.
Kinachowafurahisha ndani ya ndoa yao
“Tukiwa ndani ya ndoa tulifurahi sana siku tuliyofanikiwa kupata mtoto wetu wa kwanza, Jason, na mpaka leo tunamshukuru Mungu kwani amekua na anaendelea vema.
Matatizo wanayokutana nayo
Matatizo wanayokumbana nayo ni sehemu ya kuishi, kwani wanaishi mbali na mji na wamekuwa wakifanya kazi zao za muziki ambapo mwanamke anaimba na kundi lake la Survivor Sisters linaloundwa na wasichana walemavu watatu. Mume anaimba kama ‘solo artist’ akiwa kwenye bendi ya muziki ya Tunaweza. Hivyo kutokana na umbali, wakati mwingine wamekuwa wakifika nyumbani usiku sana kutokana na kutembea kwa shida.
“Sisi yote tunaweza kuvumilia ila tatizo kubwa ni nyumba ya kuishi ambayo huwa ni lazima kuwe na mazingira yanayoendana na mke wangu, kwa sababu hali aliyonayo si ya kushea choo hasa sehemu zile ambapo huwa kinajengwa juu kwani kama hana mtu wa kumsaidia kumpadisha inakuwa ni tatizo.
“Kwa ujumla kwa yule aliye na nyumba ambaye anaweza kutupa tukaishi tutamshukuru sana na tutafanikiwa kufanya mambo makubwa ya maendeleo kwani mimi ninao uwezo wa kufanya kazi na mke wangu. Kupitia muziki tunaweza kuendesha maisha yetu,” alisema Six.
Aliendelea kueleza kuwa mkewe na kundi lake wametoa wimbo wao unaoitwa Binuka-Binuka ambao uko mtaani na wanaomba watu waupokee na kuwapa kipaumbele