Mzee Kisumo alitoa onyo hilo wiki iliyopita katika
mazungumzo maalumu aliyofanya na Mwananchi nyumbani kwake Dar es Salaam
kuhusu kumbukumbu ya miaka 14 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere
inayoadhimishwa leo.
Alisema tatizo kubwa la chama hicho ni kwamba
kimemeendelea kuwa chama dola kikikaa mbali na wananchi, huku
kikishindwa kuidhibiti rushwa na kuwajibisha wahusika wa vitendo hivyo.
“Chama kimebaki kuwa cha walalamikaji, kila mtu
amekuwa mlalamikaji. Hata Waziri Mkuu amegeuka mlalamikaji. Sijaona watu
wanaowajibishwa kwa ufisadi,” alisema Kisumo na kuongeza:
“CCM haiwezi kujivunia ufisadi unaoonekana nchini.
Siwezi kusema imeukumbatia, lakini nasema imekuwa CCM bubu, hata
kuukemea ufisadi haiwezi. Utamaduni huu enzi za Mwalimu Nyerere
haukuwapo.”
Alisema kutokana na udhaifu huo wa CCM, kuna
uwezekano mkubwa wa chama cha upinzani, na hasa Chadema kutumia mwanya
huo kuwashawishi wananchi na kushinda uchaguzi.
Kisumo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini wa CCM, alisema ingawa Chadema haijaonyesha wazi mambo
kinayoyapigania, kinaweza kutumia agenda ya ufisadi na matumizi mabaya
ya rasilimali za umma kuwavutia wananchi na kuchaguliwa.
Alitoa mfano wa tuhuma za baadhi ya viongozi wa
Serikali kuficha mabilioni ya shilingi kwenye benki za Uswisi, kuwa
zinaweza kuwa kete muhimu ya kuwaingiza Chadema madarakani, iwapo
Serikali ya sasa haitawashughulikia wahusika.
“Wakijitokeza na kuwataja majina wahusika,
wakasema fulani na fulani ndiyo wenye mabilioni haya Uswisi, na Serikali
ikasita kuwachukilia hatua, wakasema tukiingia madarakani tutawakamata,
wananchi wanaweza kuwaamini na kuwachagua,” alisema na kuongeza:
“Wakishinda uchaguzi hata kwa viti vichache tu, watakosa nguvu bungeni,
lakini kwa wananchi watakuwa na nguvu sana.
Hii inaweza kuwasaidia kwa miaka mitano ya kwanza.
Wanaweza kupata ushindi mkubwa zaidi kwa mara ya pili na wakiingia
madarakani watawafunga viongozi wa zamani kweli.”
Mzee Kisumo anasistiza, “Hili linawezekana.
Anayesema uwezekano wa CCM kushindwa haupo, anajikana mwenyewe. CCM
inabidi ijihami na majibu ya jinsi inavyotumia rasilimali za nchi.”
Alionya kuwa si vizuri kuishia kujinadi kwa mambo
mengi mazuri iliyofanya huko nyuma, akitolea mfano kuwa hiyo ni sawa na
nguo nyeupe ambao ikiingia doa moja tu inakuwa haitamaniki tena.