Oktoba 14 ya kila mwaka imetengwa katika Tanzania kuwa siku ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Katika kukumbuka siku hiyo Mwandishi Wetu, Exuper Kachenje amefanya mahojiano na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mwaka wa Mwalimu Nyerere kwa miaka mingi, ambapo anaeleza mambo mbalimbali kuhusu miaka 14 ya Tanzania bila kuwepo kwa kiongozi huyo.
Swali: Kwa miaka 14 tangu Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere, amefariki dunia, ukiwa mmoja wa watu waliokuwa karibu
naye, ukiwa Katibu Myeka wake, Je, unahisi kukosa nini kutoka kwake?
Jibu: We, akitutoka baba yako inakuwaje?
Akiondoka, kama binadamu unakosa mtu mwenye ubinadamu, aliyekuwa
kiongozi wako na wewe msaidizi wake, unamkosa.
Kwangu, Nyerere alikuwa baba, mwalimu na Baba wa
Taifa. Tungefurahi kama angeendelea kuwa nasi leo hata kama angekuwa
kikongwe kiasi gani au hana meno;
Ninakosa staili yake ya utendaji, uwezo wa
kufikiri, kutenda, kueleza mambo kwa ufasaha na usahihi wa kiwango
kikubwa. Hivyo, tunakosa mawazo ya msingi kama kuheshimu utu wa watu
wote na usawa wa watu.
Swali: Binafsi umechota nini kutoka kwake na unakitumiaje?
Jibu: Nimechota uadilifu, ukweli, heshima kwa watu
wote, kujali watu na kujitahidi kuwa mtu kwa watu wengine. Mwalimu
alikuwa ‘role model’ (mtu wa mfano) wangu. Kitu ambacho sikuweza kuchota
kutoka kwake, ni imani yake katika utu na usawa kwa wote, niliona imani
hiyo na iliendana na imani yake katika kumcha Mungu na jitihada zake
kuhudumia watu kadri ya imani yake ya Kikristo.
Mwalimu alikuwa mtu mwenye kuona mbali, alipenda
umoja, amani kubwa na ndogo, mwadilifu, mtu maalumu aliyetumia muda wake
wote kutumikia watu wengine.
Tunaweza kusema, sisi tunajitahidi kufuata yake, lakini hatujamfikia bado tuna upungufu.
Swali: Unapozungumzia upungufu, unaitazamaje Tanzania ya leo ukiwianisha na mambo aliyoasisi?
Jibu: Yapo mengi mazuri yaliyoendelezwa na sisi
tuliobaki na viongozi wetu, moja ni Utanzania umeendelezwa. Tumedumu
kama Watanzania tukiwa wamoja na ukisikiliza Watanzania hao wanapenda
taifa lao, wanapenda umoja wao, wanapenda amani yao, wanataka uhuru wao,
wanapenda mali zao zikubalike na zitambuliwe kuwa zao.
Wanapenda viongozi wao wajue kwamba ni viongozi wa
watu na wajali wananchi, lakini hatujawa na viwango vya kukosa amani na
kuyumbisha nchi yetu.
MWANANCHI
MWANANCHI