Na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto
vimeendelea kushika kasi katika baadhi ya maeneo hususani vijijini,
licha ya Serikali na asasi mbali mbali kulipigia kelele ambapo hivi
karibuni Baba mmoja aliamua kuuza nyumba ikiwa na watoto ndani na
kutokomea kusikojulikana na kuwaacha wasijue la kufanya.
Mkasa huo wa ajabu ulitokea katika
kijiji cha Hatwelo, Kata ya Ijombe Mbeya Vijijini ambapo Mkazi huyo
aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Yuta alipouza nyumba yake na
kutokomea yeye na mkewe na kuwaacha watoto wawili wenye umri kati ya
miaka 9 na 11 wakikosa mahala pa kuishi.
Akizungumzia sakata hilo kijijini hapo,
Mwanaharakati wa haki za Binadamu, Yasin Yuta, alisema majirani
waligundua baada ya kusikia kelele za mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina
la Erasto Emmanuel (11) aliyekuwa amefungiwa ndani na kukaa kwa siku
saba.
Alisema baada ya kumfungulia mtoto huyo
ndipo ilipobainika kuwa nyumba hiyo ilikuwa imeshauzwa huku mtoto akiwa
ndani na ndipo mnunuzi alipofunga na kufuli bila kujua kama kuna mtoto
ndani huku watoto wengine wakiwa kwa ndugu zao ambao pia hawakuelezwa
kama nyumba imeuzwa.
Nyumba hiyo iliuzwa kwa Dati Nsagaje
kwa gharama ya shilingi 750,000/= ikiwa ni nyumba mbili pamoja na
kiwanja ambapo mnunuzi huyo alilipa kianzio cha shilingi laki nne
biashara iliyofanyika tangu April 26 mwaka huu na kiasi kilichobaki
wakiwa wameahidiana kulipana Mwezi Mei 15, Mwaka huu.
Wahanga wa tukio hilo ambao ni watoto
walisema hawakuwa na taarifa zozote za kuuzwa kwa nyumba wanayokaa
ambapo walisikia kuwa baba yao ameenda Sumbawanga kumfuata mke wake
ambaye inasemekana aliolewa na mwanaume mwingine.
“ Nilikuwa nimelala ndani ambapo
nilipoamka asubuhi nilikuta mlango umefungwa kwa nje hata hivyo
nilivumilia hadi njaa ilipoanza kuniuma baada ya siku tano nikaanza
kupiga kelele ndipomajirani walipokuja kunifungulia na kuniambia nyumba
imeuzwa” alisema mtoto Erasto Emmanuel.
Mtoto mwingine aliyetelekezwa ambaye
siku ya tukio alikuwa ameenda kulala kwa bibi yake Groli Emmanuel (9)
ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Hatwelo alisema siku akiwa
anaondoka aliagwa na baba yake ambaye alimwachia shilingi 3000 lakini
hakumwambia kama nyumba imeuzwa.
Kutokana na kitendo hicho
kutokukubalika,baadhi ya majirani walisema ni kitendo cha kinyama na
hakipaswi kufumbiwa macho ambapo waliamua kuchanga fedha ili kuikomboa
nyumba ili irudi mikononi mwa watoto.
Majirani hao walifanikiwa kuchanga
shilingi 410,000/= alizokuwa amedai mnunuaji ili aweze kurejesha nyumba
ikiwa ni fedha alizokuwa ametoa awali hivyo kukubaliana kuicha nyumba
hiyo ambayo kwa mujibu wa majirani na baadhi ya ndugu wamesema itakuwa
ni mali ya watoto.
Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya
kawaida na kuonesha kukosa uwajibikaji kwa baadhi ya viongozi wa
Serikali ya Kijiji ambao walishiriki moja kwa moja zoezi hilo huku
wakiwa wamesaini kama mashahidi na kugonga mhuri wa Serikali ya Kijiji
walipoulizwa kuhusiana na sakata hilo hawakuwa na majibu ya kuridhisha.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Hawelo,
Ibrahimu Mponzi, alisema kitendo alichokifanya muuzaji ni cha kawaida
kwa sababu ameuza mali yake mwenyewe na kwamba wao kama majirani na
serikali ya kijiji hawawezi kuhoji atakako waacha watoto kwa sababu ni
mipangilio ya maisha ya kila mtu.
Mbali na mwenyekiti wa Kijiji kuwa
shahidi wa upande wa mnunuaji akiwa sambamba na watu wengine wanne
akiwepo Mkewe ambaye pia ni Balozi wa nyumba kumi pia waliosaini wengine
ni ndugu wa mnunuaji ili hali muuzaji akiwa hana shahidi hata mmoja.
Aidha juhudi za majirani kuikomboa
nyumba hiyo na kuwa mali ya watoto zilifanikiwa ambapo mnunuzi Datistani
Mwanshinga alibatilisha ununuzi wa nyumba hiyo Mei 9, Mwaka huu baada
ya kukiri kurejeshewa fedha zake.