Home » » AFYA :JE UNAFAHAMU KIUNDANI UGONJWA WA PUMU (ASTHMA) NA DALILI ZAKE...

AFYA :JE UNAFAHAMU KIUNDANI UGONJWA WA PUMU (ASTHMA) NA DALILI ZAKE...

Utangulizi Ugonjwa wa pumu ni ugonjwa sugu ambao huathiri njia za hewa ambazo huingiza na kutoa hewa katika mapafu. Upatapo ugonjwa wa pumu, kuta za ndani za njia ya hewa hupata maumivu (inflammation) na kuvimba. 

Maumivu katika njia za hewa huzifanya kujihami kwa kusinyaa na hivyo kupunguza kiasi cha hewa kinachopita kwenda kwenye mapafu. Hali hii husababisha muathirika kutoa mlio kama wa filimbi au mluzi wakati wa kupumua. 




Pumu husababishwa na nini? 

Bila shaka mpenzi msomaji umekua ukijiuliza swali hili mara kwa mara. Haifahamiki haswa ni sababu zipi zinazopelekea njia za hewa kupata maumivu na hivyo kupelekea mtu kupata pumu. 

Vyanzo mbali mbali vinaonyesha kuwa inatokana na mseto wa vitu kama tumbaku, maradhi na baadhi ya vizio

Pia kuna vitu katika mazingira ambavyo vinaweza kusababisha mtu kushambuliwa na pumu. Vitu kama vile mazoezi, vizio, viwasho (irritants) na maradhi yatokanayo na virusi. 

Baadhi ya vizio ni kama vifuatavyo: 

-Vumbi 
-Mende 
-Chavua (pollen) kutoka kwenye miti na majani 
-Magamba ya wanyama, manyoya n.k 

Viwasho kama: 
-Moshi wa sigara 
-Uchafuzi wa hewa 
-Harufu kali (kutoka kwenye rangi au chakula) 
-Msongo wa mawazo 
-Dawa kama Aspirin 
-Ugonjwa wa kucheua 
-Viwasho au vizio vitokanavyo na kemikali 
-Magonjwa ya njia ya hewa n.k.

Ieleweke kwamba orodha iliyotajwa hapo juu siyo kamilifu kwa maana kwamba haijasheheni vitu vyote vinavyoweza kuleta dalili za pumu na pia muathirika anaweza kuathirika na kimoja wapo au zaidi. 

Vigezo hatarishi 

Baadhi ya vigezo hatarishi vinavyoweza kuongeza uwezekano wa kusababisha ugonjwa wa pumu ni pamoja na: 

-Kuishi katika miji mikubwa, haswa katikati ya mji ambapo huongeza uwezekano wa kukutana na vizio 

-Kuvuta hewa iliyo na moshi 

-Kemikali zitokanazo na kilimo, dawa za kutengeneza nywele, rangi, vyuma, plastiki au vifaa vya elektroniki 

-Kuwa na mzazi mmoja au wawili wenye pumu 
-Kuathirika na maradhi ya mfumo wa hewa kama kikohozi na mafua wakati wa utoto. 

-Unene wa kupita kiasi (obesity) 

-Ugonjwa wa kucheua na kiungulia (Gastro esophageal reflux disease) 

Dalili za Pumu 

Baadhi ya dalili za kawaida za ugonjwa wa pumu ni kama zifuatazo: 

-Kikohozi: Mara nyingi kikohozi cha pumu huwa kikali nyakati za usiku au alfajiri na hivyo kumfanya mwathirika kutolala vizuri 

-Kutoa sauti ya mfano wa mtu anayepiga mluzi au filimbi wakati wa kupumua 

-Kifua kubana: Mgonjwa husikia kama kitu kinakandamiza kifuani au wakati mwingine husikia kama mtu amemkalia kifuani. 

-Kukosa hewa: Baadhi hujisikia kama hawawezi kupumua na kukosa hewa ya kutosha inayoingia au kutoka kwenye mapafu. 

-Kupumua haraka haraka 

Ikumbukwe kwamba si watu wote huwa na dalili zilizokwisha tajwa hapo juu na dalili zaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu. 

Dalili pia zinatofautiana ukali. Wakati kwa mwingine dalili zinakuwa za wastani, wengine zinakuwa za kukera tu au mbaya kiasi cha kumzuia muathirika kufanya shughuli zake za kila siku. 

Vile vile wapo wengine ambao dalili zinakuwa mbaya kiasi cha kuhatarisha maisha. Dalili pia zaweza kutofautiana kwa kipindi zinapotokea. 

Wengine hupata dalili mara moja tu kwa mwezi, wengine kila wiki na wengine hupata dalili kila siku. Hata hivyo iwapo muathirika atapata matibabu sahihi anaweza kuishi na dalili chache au bila dalili kabisa. 

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger